Mwambesi, Ruvuma – Juni 2025
Wawakilishi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), pamoja na Ofisi ya Makamu wa Rais, wamefanya ziara ya ukaguzi katika Hifadhi ya Mazingira Asilia ya Mwambesi, Wilaya ya Namtumbo, Mkoa wa Ruvuma, ili kufuatilia utekelezaji wa Mradi wa Kuimarisha Ustahimilivu wa Bioanuwai ya Misitu ya Mazingira Asilia dhidi ya Matishio ya Mabadiliko ya Tabianchi.
Katika ziara hiyo, wajumbe wametembelea eneo la ujenzi wa jengo la utalii, jengo la ulinzi, pamoja na geti la kuingilia hifadhi, ambapo mradi huo tayari umeanza kutekelezwa na umefikia asilimia 10 ya kazi yote. Mradi unatekelezwa chini ya usimamizi wa Brakel Company Ltd kwa gharama ya Shilingi milioni 211, na unatarajiwa kukamilika ifikapo tarehe 25 Oktoba 2025.

Akizungumza wakati wa ukaguzi huo, Mkuu wa Manunuzi kutoka TFS Makao Makuu, Bw. Fridolin Matembo, alisema:
“Tunaipongeza kampuni kwa kuanza vizuri kazi hii. Kasi ya awali ya ujenzi imeridhisha, lakini tunasisitiza iongezwe ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.”
Mradi huu wa Bioanuwai ni sehemu ya jitihada za pamoja kati ya Serikali ya Tanzania kupitia TFS na Ofisi ya Makamu wa Rais, kwa kushirikiana na UNDP na ufadhili wa Mfuko wa Mazingira wa Dunia (GEF). Unalenga kuimarisha miundombinu ya uhifadhi, kuboresha huduma za misitu kwa jamii, na kuchochea utalii wa kiikolojia katika maeneo ya hifadhi ya asili.
