Latest News

  • Home
  • stories
  • mradi-wa-bioanuwai-waendelea-kuimarisha-miundombinu-ya-uhifadhi-pindiro-yapata-vifaa-na-maendeleo-ya-ujenzi

MRADI WA BIOANUWAI WAENDELEA KUIMARISHA MIUNDOMBINU YA UHIFADHI – PINDIRO

Kilwa, Lindi – Juni 2025

Kamati ya Utekelezaji wa Mradi wa Kuimarisha Ustahimilivu wa Bioanuwai ya Misitu ya Mazingira Asilia dhidi ya Matishio ya Mabadiliko ya Tabianchi kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), imefanya ziara ya kikazi katika Hifadhi ya Pindiro, Wilaya ya Kilwa, Mkoa wa Lindi, kwa lengo la kukagua maendeleo ya ujenzi wa miundombinu ya uhifadhi pamoja na kukabidhi vifaa vya kazi.

Mradi wa ujenzi unaoendelea ndani ya hifadhi hiyo umefikia asilimia 46, ukihusisha jengo la utalii, vyoo, jengo la mlinzi, na geti la kuingilia, kwa gharama ya Shilingi milioni 297, chini ya mkandarasi Strider Engineering Ltd. Mradi huo unatarajiwa kukamilika Oktoba 2025.

Mhandisi Hendry Sanga, ambaye ni mkandarasi wa mradi, alisema kazi inaendelea vizuri na wanaendelea kuzingatia muda wa makubaliano pamoja na ubora wa kazi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Manunuzi kutoka TFS, Bw. Fridolin Matembo, alisema:

“Tunaipongeza kazi nzuri inayofanywa na mkandarasi. Kasi ya utekelezaji ni ya kuridhisha, na tunasisitiza kwamba mradi huu ukamilike kwa muda uliopangwa na kwa viwango vya ubora vinavyokubalika.”

Katika hatua nyingine ya ziara hiyo, pikipiki mbili zimekabidhiwa rasmi kwa hifadhi hiyo, ikiwa ni sehemu ya vifaa vya kazi vilivyotolewa na UNDP kusaidia shughuli za uhifadhi.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mratibu wa Mradi, Bw. Mteleka Someni Lusugu, alisema:

“Pikipiki hizi mbili ni sehemu ya vifaa muhimu ambavyo UNDP ilikabidhi kwa Mheshimiwa Waziri wakati wa uzinduzi wa mradi kule Pugu Kazimzumbwi. Zinaletwa Pindiro kusaidia uratibu wa kazi za uhifadhi na kuongeza ufanisi kwa maofisa wetu walioko kwenye maeneo ya kazi.”

Mradi wa Bioanuwai unatekelezwa kwa miaka sita katika maeneo mbalimbali ya misitu ya asili nchini, ukiwa na lengo la kuimarisha usimamizi wa rasilimali misitu, kuongeza ustahimilivu wa jamii dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi, pamoja na kuboresha miundombinu na huduma za uhifadhi kwa maendeleo endelevu ya wananchi na taifa.